DADA LAKINI UNAJUA BABA ALINIBAKA?

Nilishasema siwezi tena kuajiri mfanyakazi wa ndani, tabia za mume wangu kutembea na wafanyakazi wa ndani zilinilazimisha hata kuacha kazi ili nisiwe na sababu ya kuajiri mfanyakazi na kufanya kila kitu mwenyewe.
Niliamua kuwa Mama wa nyumbani ili tu kulinda familia yangu, watoto wangu wawili wadogo wa mwisho niliwalea mimi mwenyewe, hii ni baada ya mume wangu kutembea na wafanyakazi wa ndani watano, wawili akiwapa mimba na kutoa na mmoja kumzalisha kabisa.
Nilijua mume wangu hawezi kuacha hiyo tabia kwani kila siku aliomba msamaha na nikimsamehe alirudia tena. Lakini nikiwa nimeshamaliza kabisa kuzaa, Mungu akinijaalia watoto wane nilijua nimemaliza, ghafla nilijistukia nina ujauzito.
Mwanzoni sikujua kwani nilipokosa siku zangu nilijua kuwa ni uzee umekaribia, miaka 45, mtoto wangu wa mwisho akiwa na miaka 8 sikuwaza kabisa kwamba nitakuja kuzaa tena.
Hivyo nilipoanza kuumwa nilijua ni homa za kawaida na kichefuchefu cha kawaida, mpaka dalili zilipozidi nikaamua kwenda kupima na kuambiwa nina ujauzito wa miezi mitatu.
Sikua na hata wazo la kutoa, nilipomuambia mume wangu aliniambia nimipango ya Mungu hivyo tuzae tu, lakini mimba hii ya uzeeni ilinisumbua sana, mara kadhaa nililazwa hospitalini nikiamrishwa kupumzika hivyo nikalazimika kutafuta mfanyakazi.
Kwangu hili lilikua gumu sana, kwani nilikumbuka tabia ya mume wangu lakini nilijipa moyo kuwa kashakua mtu mzima kwani ana watoto wakubwa tena wakike, mtoto wetu wa kwanza akiwa kidato cha pili mwenye umri wa miaka 16.
Lakini kwa tahadhari niliamua kutafuta kabinti kadogo ambako niliamini hata hatakatamani, niliongea na Mama mabaye alinitafutia mfanyakazi kutoka Kijijini singida, huyu ndiyo alikua amemaliza darasa la saba na kufaulu vizuri tu.
Alishindwa kwenda shule kwasababu mbili, kwanza alifaulia mbali, Kilakala Morogoro shule ya watu wenye vipaji maalum, kwa maana hiyo gharama za kumpeleka zilikua kubwa na wazazi wake hawakua na uwezo.
Lakini pili alikua na pacha wake wakiume ambaye yeye alifaulia shule ya kata hivyo wazazi wakaamua asome mwanaume na si mwanamke. Hivyo walivyosikia suala la ajira hawakujiuliza mara mbili, ilibidi kufanya kazi ili aweze kumsomesha pacha wake.
Binti yule ambaye alikua ndiyo ana mikaa 14 alikuja kwangu bado kadogo, hata kuvunja ungo bado, hata matiti hayajaota vizuri. Pamoja na udogo wake alikua akifanya kazi kwa bidii, alikua na akili sana kuliko hata binti yangu ambaye alikua akisoma bweni.
Jioni aliwafundisha watoto wangu wengine wadogo waliokua wanasoma shule za msingi na mara nyingi alichukua vitabu vya binti yangu na kujisomea. Lengo lake lilikua ni kutafuta pesa ili afike chuo kikuu, alikua na ndoto zakuwa Daktari na alijua kama akifanya kazi vizuri na kumsomesha pacha wake basi akiwa tajiri naye atamsomesha.
Hakuwaza kuhusu umri kwamba atakua na umri gani kipindi hicho, lakini nilimpenda kwani mbali na nidhamu na kufanya kazi vizuri maendeleo ya wanangu shuleni yalibadilika, alikua kama Dada yao akiwafundisha na kuwasimamia alipenda sana kuwafundisha. Nilijifungua na mtoto akiwa na mwaka mmoja ndipo nilianza kuona mabadiliko.
Kwanza binti wawatu alikosa raha, alikua ni mtu wa kujikunyata tu, kila wakati akijifungia kulia, akiwa muogamuoga na alipokua akimuona mume wangu nilimuona kabisa akitetemeka kwa uoga, nilihisi kitu na nilianza kupata wasiwasi hivyo nilichunguza.
Siku moja usiku nilimsikia mume wangu akiamka, nilijua ataelekea chooni lakini alifungua mlango na kutoka. Nilinyanyuka na kumfuatilia, aliingia kwenye chumba cha yule binti wa kazi, sikutaka kusikiliza nilijua mchezo umeanza hivyo ilikua imebaki kumfukuza tu yule binti.
Asubuhi ya siku iliyofuata binti wawatu akiwa hajui chochote nilimuambia afungashe mizigo yake aondoke. Kwanza alikua anatembea na mume wangu na pili nilikua simhitaji tena kwani mtoto alishakua mkubwa.
Binti alishangaaa, alianza kuomba msamaha bila kujua kosa lake, sikutaka kumuambia sababu ya kumfukuza, sikutaka ajue kuwa najua mume wangu anamfanyia ushenzi wa namna ile. Niliona aibu kwani yule binti alikua ni mdogo kabisa kuliko hata mtoto wangu wa kwanza.
Najua ningemuambia najua basi angeweza kuongea na ikawa aibu ya Baba wa miaka hamsini kutembea na binti wa miaka 15. Kwa cheo cha mume wangu ingemharibia na kuharibu maisha yetu wote. Binti alilia na kuomba msamaha lakini sikujali nilimuambia sihitaji mfanyakazi tena na aondoke.
Wakati nikiendelea kumsihi binti alidondoka chini na kupoteza fahamu, nilijua anaigiza mpaka nilipomwagia maji hanyanyuki, harakaharaka nilimpakia kwenye gari na kumpeleka hospitalini. Kule alipimwa kila kitu na madaktari kuniambia ana mimba ya miezi miwili.
Kuseama kweli nilishangaa kwani binti hata bado alikua hajaanza kuona siku zake, alikua amechelewa sana kuvunja ungo na hata bado alikua hajawa na ule muonekano wa mwanamke. Alipewa zile habari na kubaki kulia tu.
Nilimuondoa harakaharaka hospitalini kwani sikutaka ahojiwe, nilijua kama nikiruhusu kuongea na mtu atamtaja mume wangu na mume atafungwa. Nilimrudisha nyumbani nikiwaza namna ya kumtoa ile mimba.
Nyumbani sikutaka hata kumbana aniambie mimba ni ya nani, nilishajua hivyo sikutaka hata anyanyue mdomo kwani wanangu wengine wangesikia. Nilianza mikakati ya kumtoa ile mimba, nilimtoa na kutoka naye sehemu kisha nikamuambia anatakiwa kuitoa.
Yaani kama mtu mzima, alianza kuniambia madhara ya kutoa mimba na kuniambia mbali na kuogopa kufa lakini ile ilikua nidhambi, aliniuliza swali “Dada hivi mtu akija na kukuambia amuue Jack wewe utakubali?” Jack ni mtoto wangu wa kwanza, niliishiwa pozi na kujikuta sina chakusema.
“Dada huyu ni mwanangu, ameshakuwa mkubwa ameshakua na roho…” Alianza kunielezea sayansi ya namna mtoto anavyokua tumboni mpaka akaanza kuniboa, nilitamani kumpiga nikiwaza kwanini Mungu alimpa akili zote hizi, angekua mjinga mjinga kama wale wnegine si angetoa tu.
Niliamua kumgeuzia kibao, nikamtukana na kumpiga nikimuambia alitembea na mume wangu, nilimtisha na kumuambia nilazima atoe au namrudisha kijijini. Hapo ndipo alinywea kidogo, nikama alikua hataki kurudi kijijini kwani alijua ndoto zake za kusoma zitayeyuka.
“Dada lakini unajua Baba alinibaka? Mimi sikupenda alinibaka na kila siku usiku anakuja kunibaka, anaseama kuwa nikiongea ataniua mimi na ndugu znag, ananionyesheaga bastola ndiyo maana sipigi kelele” Aliongea kwa sauti ya chini, hapa alionyesha huruma, huku machozi yakimtoka, kidogo nilimuonea huruma.
Lakini ilikua ni lazima nitilie mkazo ili aitoe ile mimba. “Kesho nakupeleka kutoa mimba, kama hutaki nakurudisha kijijini kwenu na mimba yako tuone kama utasoma tena, kama Baba yako hatakuua, nibora utoe uendelee na kazi…”
Nilimtishia huku nikiondoka, nilimucha palepale kwani haikua mbali sana na nyumbani. Alirudi kwa miguu huku akiwa na mawazo mengi, hata chakula hakula akijifanya kua naaumwa. Watoto walitaka kujaua naumwa nini lakini niliwafokea wamuache.
Usiku sikulala, niliwaza kuwa akitoa tu ile mimba namuondoa, simuachi hata akarudi nyumbani. Wakati nikiwa katika mawazo yangu, mume wangu aliamka, nilimuona akitembea kwa kunyata mpaka kwenye chumba cha yule binti, aliingia na kama kawaida sikutaka kujua kinachoendelea.
Nilirudi na kitandani na kuanza kulia kua huyu ni mwanaume gani. Alimaliza ujinga wake huko na kurudi chumbani, kweli niliumia sana, maneno ya yule binti “Unajua Baba alinibaka…” yalijirudiarudia kichwani mwangu. Huyu ni mwanaume gani, niliwaza, lakini mimi ndiyo nimemlea kuwa hivi.
Niliumia sana na kitendo nilichokua nikitaka kumfanyia yule binti, kumtoa mimba na kumfukuza, niliona sio haki hivyo nilitaka akitoa ile mimba basi nammpeleka Mwanza kwa mdogo wangu, aishi huko na nitamsomesha afikie malengo yake ya kuwa Daktari.
Lakini bado nilitaka atoe ile mimba kwani kubaki nayo ingekua aibu. Asubihi kama kawida nilichelewa kuamka, nikijua binti yupo atafanya kila kitu, lakini mpaka saa mbili wakati huo wanangu washaenda shule na mume kaenda kazini alikua bado hajaamka.
Niliingia chumbani nikafungua mlango hakukua na mtu, nilitaka kutoka lakini nilihisi kitu nilitudi chumbani na kuangalia, macho yalitua juu kwenye feni ya juu. Mwili wa binti ulikua ukininginia, alichukua meza na stuli, akapanga viti.
Akatafuta kamba ya katani stoo na kisha akajitundika. Nilijikuta na changanyikiwa, nilipapasa papasa macho na kuangalia pembeni kulikua na kikaratasi kimendikwa.
“Dada mimi nimechoka, Baba kanibaka tena, hata nikitoa mimba ukanisamehe ataendelea kunibaka tena na nikirudi nyumbani na mimba Baba ataniua, mimi nilitakiwa nimsomeshe pacha wangu lakini nimebeba mimba, nisamehe Dada yangu nimeamua kufa na mwanangu”.
Nilidondoka chini na kuanza kulia, maneno yake yaliniumiza, yalijirudia kichwani. “Dada unajua lakini Baba alinibaka…” nilikificha kile kikaratasi kwani sikutaka mtu akione. Niliita majirani amabo waliita Polisi na mwili kuchukuliwa.
Mchana mume wangu alirudi baada ya kumpigia simu, alijifanya kusikitika kwa kilichotokea, nilijikaza na kujifanya sijui chochote, mwili ulipelekwa kijijini na binti alizikwa, mpaka sasa bado najiona muuaji, nisingemlinda mume wangu, kumvumilia kwa tabia yake binti wa watu labda angekua hai sasa.
Nipona mume wangu lakini naogopa hata kumgusa, niko njiapanda sijui hata nifanyeje, natamani kuamuambia ukweli na kumuacha lakini nitaenda wapi na umri huu sina hata senti kumi, nimechanganyikiwa na kila siku maneno ya yule binti yanajirudia kichwani kwangu “Dada Lakini Unajua Baba Alinibaka…”
***MWISHO.***

Leave a Reply