MAPENZI… MCHEZO WA HATARI

Inawezekana utasema nilikuwa fala na mwingine akasema kwamba nilikuwa mjanja. Kuna msichana namkumbuka kichwani mwangu, jina lake aliitwa Amina Saidi. Alikuwa msichana mrembo kwa sura, umbo na vitu vingine ambavyo msichana wa kisasa alitakiwa kuwa navyo. Mara ya kwanza kukutana naye ilikuwa katika Chuo cha Ustawi kilichokuwa Mwenge jijini Dar es Salaam. Nakumbuka alikuwa akisubiri daladala kituoni, magari yalikuwa shida mno kwani mataa ya pale Sayansi yalizuia kabisa magari kupita. Nilipomuona, sikutaka kuchelewa, nikalisogeza gari na kushusha kioo, nikaanza kumwangalia. Kwanza sikuamini kama Tanzania tulikuwa na mrembo kama alivyokuwa Amina, kila nilipomwangalia, alinivutia mno. Nikapiga honi, Amina akayageuza macho yake na kuniangalia, nikamuita kwa kutumia mkono wangu, akaja na kuinamia dirisha la gari langu. Alikuwa msichana mpole mno ambaye mara kwa mara uso wake ulikuwa na tabasamu pana lililonichanganya kupita kiasi. Watu wote waliokuwa kituoni hapo, wakaanza kumwangalia. Kuna wengine walikuwa wakimuonea wivu kwa sababu aliitwa na mimi, mtu mwenye gari lakini kuna wengine walionekana kuchukizwa. “Mambo,” nilimsalimia huku nami nikiliachia tabasamu liutawale uso wangu. “Poa.” “Unakwenda wapi?” nilimuuliza. “Nakwenda Kagera.” “Ok! Naweza kukusaidia mana’ke mi’ mwenyewe nafika Magomeni,” nilimwambia japokuwa kiukweli siku nikienda Magomeni. “Sawa. Nitashukuru sana.” Nikamfungulia mlango na mtoto mzuri kuzama ndani. Sketi yake iliishia magotini, hivyo alivyokaa kitini tu, ikapanda na kuyaacha mapaja yake wazi. Nilichanganyikiwa, Amina alinidatisha kupita kawaida. Wakati mwingine nilikuwa nikiyaangalia mapaja yake kwa matamanio makubwa, sikutaka kuuficha ulijari wangu. Mapaja yake yalikuwa meupe mno yasiyokuwa na doa, nilivuta picha kipindi ambacho ningemchukua na kumpeleka chumbani kwangu na kumlaza kitandani, nikafikiria maisha ya raha ambayo ningekuwa nayo ndani ya dakika chache, hakika tamaa ikaniwaka. “Umependeza,” nilimwambia huku uso wangu ukiwa kwenye matamanio. “Asante sana.” Muda wote nilikuwa nikiomba Mungu tukutane na foleni kubwa. Sijui kama ni Mungu au shetani alikuwa ameisikia sala yangu, tulipofika Sinza Mori, kulikuwa na bonge la foleni, nikatamani kushangilia, hapo nikapiga breki na kuanza kupiga naye stori. “Samahani, unajua ni kosa la jinai kuongea na mtu usiyemfahamu japo kwa jina, unaitwa nani?” nilimuuliza huku nikitabasamu. “Naitwa Amina.” “Waoooo!! Unasoma au unafanya kazi?” “Nasoma hapo Ustawi, mwaka wa kwanza,” aliniambia. Sikutaka kujua anasomea nini, sikuwa professa au mzazi wake, nilichokuwa nikitaka kujua ni vitu vichache tu ambavyo nishavijua. Amina akajiachia kitini tena huku akiwa amevua viatu na kuiweka miguu yake katika dashboard ya gari. Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wangu na Amina kufahamiana, baada ya hapo, nikawa nikimpigia sana simu, wakati mwingine wakati nakwenda ofisini, namfuata nyumbani kwao na kumuacha chuoni kwani hakukuwa mbali na ofisini kwangu. Kadri siku zilivyozidi kwenda mbele, nilimuona Amina akivutia sana, mavazi yake ya kimitego aliyokuwa akiyavaa yalinichanganya mno. Mtu mzima nikajitahidi kuvumilia lakini nikaona wapi, nilichokifanya ni kupanga naye miadi ya kuonana naye, akakataa kuonana nami nyumbani kwangu, nikamwambia siyo kesi kama tukionana Jangwani Sea Breaze. Kweli tukaonana, tukala sana bata huku nikimlia timing, baada ya kumaliza kila kitu, nikamwambia tuchukue chumba, Amina akakataa katakata. Nikaona kidume mimi kushindwa kumlaghai msichana kuchukua chumba ni kosa la jinai, hapo ndipo nilipoanza kazi hiyo. Haikuwa ndogo, nilijitahidi kufanya kila kitu, akakataa, nikajaribu kumrubuni kwa vitu vingi, bado akakataa. Kiukweli nilikasirika na nilipanga kumuacha hukohuko na mimi nisepe naye kwani nilikuwa nimetumia kiasi kikubwa cha fedha, halafu alikataa kuingia nami chumbani. “Kwani demu yupo peke yake? Mbona unapendwa na wasichana wengi kuanzia mitaani mpaka ofisini, achana naye bwana, hata kama utamchunia, usichukue hatua ya kumuacha, atarudi na nani? Unajuaje kama ana nauli au hana? Ukimuacha, utamtesa sana, chukulia poa,” niliisikia sauti moyoni wangu, sikujua kama ilikuwa sauti yangu, ya shetani au ya Mungu, nikakubaliana nayo. Tulipoingia ndani ya gari, nilionekana tofauti sana, nilimkasirikia na sikutaka kuzungumza naye kabisa. Amina alikuwa tofauti, alikuwa akiongea sana lakini sikumuonyeshea sapoti yoyote ile. “Nyemo,” aliniita. “Naam.” “Mbona nazungumza peke yangu tu? Ndiyo umekasirika?” aliniuliza huku akinishika pajani. “Naomba uniache Amina,” nilimwambia kwa ukali kidogo. “Mmh! Sawa,” aliniambia. Japokuwa nilimpiga mkwara lakini hakutaka kutulia, bado aliendelea kunipigisha stori lakini nikala bati, nilipomfikisha nyumbani kwao, sikumuaga, nikapiga gia na kusepa. Amina, msichana mrembo sana, akaanza kunitafuta simuni. Kila alipokuwa akipiga simu, sikuwa nikipokea, na hata alipokuwa akiniandikia meseji, sikuwa nikimjibu. Najua aliumia ila nilitaka kumuonyeshea kwamba nilikasirika sana. “Nyemo, mbona unakuwa na hasira sana, mbona unanifanyia hivi? Mbona hukuniambia kama unataka niwe mpenzi wako na mwisho wa siku unataka tufanye mapenzi? Nyemo, mbona unakuwa katili namna hiyo? Naomba nikuulize kitu halafu tutapanga mambo mengine, unanipenda?” aliniuliza kwa kutumia meseji, nikaijibu fastafasta. “Ninakupenda, japokuwa sikukwambia lakini ninakupenda. Nilidhani kwamba matendo yangu yangeonyesha upendo nilionao kwako, naamini katika matendo zaidi ya maneno,” nilimwambia. “Sawa. Nashukuru kwa kunipenda. Naomba tuonane sehemu,” aliniambia. “Baada ya hapo nini kitaendelea? Utanipa?” “Nyemo….” “Naaam.” “Mambo mazuri hayataki haraka.” “Najua. Ila daah! Nashindwa kuvumilia.” “Najua unaumia ila samahani, tuonane wapi?” “Lini? Leo?” “Ndiyo. Wewe si unataka leo! Au hutaki leo?” “Nakata leoleo, tuonane……” nilisema lakini kabla sijamalizia sentensi yangu, akaingilia. “Nakuja kwako.” Nilihisi damu yangu ikizunguka kwa kasi mno, sikutegemea kile alichokuwa ameniambia, kwa wiki mbili mfululizo mtoto alikuwa akinizingua, mwisho wa siku, leo hii alikuwa tayari kuchinjwa, tena ndani ya chumba changu mwenyewe, katika uwanja wangu mwenyewe. “Saa ngapi sasa?” “Wewe unataka nije saa ngapi?” “Hata sasa hivi.” “Basi sawa! Nakuja.” Simu zikakatwa na kuanza kujiandaa fastafasta. Hakuna kipindi ambacho mwanaume anakuwa kwenye haraka kama kipindi hiki. Niliinuka kutoka kitandani, nikaandaa kiwanja changu kwa kuweka shuka safiiii, yaani hata lile ambalo nililiweka jana tu niliona kwamba ni chafu. Baada ya hapo, nikawasha televisheni na kuanza kuangalia. Muda uliyoyoma, hakutaka nimfuate kwa gari langu, alichukua bajaj, alipokaribia, akaniambia niende kumchukua mtaa wa juu, nikamfuata. Mzuri-mzuri tu, huwa hachuji, mtoto alipigilia hasa, alionekana kuwa mrembo sana, nilipomuona tu, hamu ya kufanya naye mapenzi ikazidi kunipanda. Kitu ambacho nilikuwa nikikifikiria ni kumvua nguo zake tu na kuanza kazi. Nikamkumbatia kwa furaha na kisha kusepa zetu nyumbani. Nilipofika, nikajifanya kama sikumbuki alichokifuata, nikaanza kupiga stori nyingine kabisa ila mwisho wa siku, nikamgusia lengo kamili, lile lengo lililomfanya kutoka kwake Kagera kuja nyumbani kwangu. “Subiri kwanza,” aliniambia, tayari pensi yangu ilikuwa pembeni kabisa. “Kuna nini tena jamani?” “Naomba kwanza tuzungumze.” “Unataka tuzungumze nini Amina, tutazungumza baadaye.” “Nyemo.” “Naam.” “Najua unanipenda, ila subiri tuongee kwanza.” “Daaah! Sawa, niambie kuna nini.” Kabla hajaanza kuzungumza alichotaka kuzungumza, machozi yakaanza kumbubujika mashavuni mwake, kwanza nikashangaa, sikuamini kile nilichokuwa nikikiona. Msichana mrembo niliyekuwa nikimpenda kwa dhati, alianza kulia, nikapiga moyo konde kwamba hata kama angejifanya kulia, mechi ilikuwa ni lazima ichezwe, yaani machozi yake niliyafananisha na mvua inyeshayo uwanjani, kamwe isingeweza kusababishwa kuahirishwa kwa mechi. Nikamsogelea na kumkumbatia, kumbatio langu lilikuwa ni la uhakika sana, sikutaka kuituliza mikono yangu, niliipitisha huku na kule hali iliyomuonyeshea kwamba leo moto ulikuwa ukiwaka ndani. “Nyemooooo….” aliniita kwa sauti ya kubembeleza. “Niambie baby…” “Sitaki tufanye mapenzi.” “Kwa nini?” niliuliza kwa kuhamaki. “Nyemo, pleaseeee, u mtu mwema sana kwangu, ni rafiki yangu mkubwa, sitaki kukupoteza, sitaki kukuua.” “Unamaanisha nini mpenzi, ndo unanibania kiaina?” “Hapana Nyemo, nimeathirika na UKIMWI, natembea na Virusi vya UKIMWI,” aliniambia. Kwanza nikashtuka, kama sikuamini kile alichokuwa ameniambia, nadhani aliishtukia hali hiyo, akachukua pochi yake na kutoa karatasi fulani na dawa na kisha kunionyeshea, kweli alikuwa muathirika wa Ugonjwa wa UKIMWI. Nikashusha pumzi ndefu, msichana huyu, Amina, alikuwa ameamua kuyaokoa maisha yangu. Alijua kwamba ni muathirika lakini hakutaka kuniambukiza ugonjwa huo kwa kuamini kwamba na mimi ningekwenda kumuambukiza mtu mwingine na kuufanya ugonjwa huu kusambaa. Kuanzia siku hiyo, Amina akawa rafiki yangu wa kawaida, kila aliyemfuata, alimwambia wazi kwamba alikuwa ameathirika japokuwa wanaume wengine walikuwa wabishi kwa kuona wanabaniwa sana. Baada ya urafiki wetu wa miaka mitano, Amina akaanza kuugua ugonjwa ule, ilikuwa ni huruma ya hali ya juu, uzuri wake ukapotea, akaanza kukonda, kukohoa na kunyonyoka nywele. Amina akabadilika kabisa, kila nilipokuwa nikimwangalia, nilikuwa nikilia mno, alinifariji sana na kuniambia kwamba kwa kutumia kipaji changu cha kuandika basi niweze kuzungumza na watu wengine kuhusu ugonjwa huu. Nakumbuka mwezi wa nne mwaka juzi ndiyo tulimzika Amina katika Makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam. Aliniachia ujumbe mzito mno, kuanza siku hiyo, nikaanza kujilinda na kuwalinda wengine huku nikitumia kipaji changu kuwaambia wengi kuhusu ugonjwa huu unaotisha. Ndugu yangu, rafiki yangu, ugonjwa huu upo, wakina Amina wapo wengi sana tena wenye roho mbaya ya kutaka kuwaangamiza hawa wakina Nyemo. Yakupasa kuwa makini. Sikwambii ufanye ila utumie kinga, hapana, nakusihi uache kabisa mchezo huo kwani starehe ya dakika moja, itakufanya kuteseka muda mwingi kitandani. Kwa walioathirika, Mungu yupo pamoja nanyi, kama unao, usitake kuusambaza, waonee huruma watu wengine.

Leave a Reply