NISAMEHE KABURI

Amakweli neno ninge huja wakati tayari tumechelewa.

Naam! Nami najikuta nasema ningejua! Japokuwa najisikia vibaya sana kutumia kauli hiyo!

Nazungumza nawe mwanangu wa pekee! Mwanangu usiyeweza kunijibu kitu chochote kile kwa sababu umenyamaza kimya, kimya cha milele.

Nazungumza nawe Jimmy huku nikijiona ni uchi mbele ya dunia nzima.

Ama kwa hakika dunia yote inanizomea, sina budi kukubaliana na matusi yote ambayo natukanwa kwa sababu nastahili.

Mwanangu Jimmy, nipo mbele ya kaburi lako. Ninasema na kaburi lako nikiamini litasema nawe.

Jimmy! Sikuwa baba mbaya kama dunia nzima inavyoniandika na kunisema. Ni upendo uliopitiliza Jimmy.

Nilifanya kazi kwa bidii sana Jimmy ilimradi nipate pesa za kutosha nawe usome kwa kiwango cha juu tena katika shule bora.

Niliyafanya haya mwanangu kwa sababu mimi sikufanyiwa na babu yako. Sikuipata elimu kabisa bali nimepata bahati tu ya kuwa na akili ya biashara.

Jimmy! Sikutaka kusikia lolote kwa wanawake waliokuwa wakikusema kuwa unawasumbua watoto wao wa kike kwa kuwatongoza kisha kuziumiza nafsi zao, wakaenda mbali zaidi na kusema kuwa unawajaza mimba na kisha unawashawishi kuzitoa.

Sikutaka kuwasikia kwa sababu nilikuwa nina chuki juu ya wanawake wote! Jimmy mwanangu si unakumbuka nilikueleza visa alivyonifanyia mama yako, sikukudanganya hata neno moja Jimmy. Mama yako alinitenda sana, hatimaye kunikimbia huku ukiwa na miaka miwili tu, akaenda kuolewa huko mjini na kijana mwenye pesa. Akaniacha nikiteseka mimi nawe!

Jimmy, ningeanza vipi kuwapenda wanawake!! Nilijua wanakuonea wivu kwa sababu tu walau umepata baba anayekupenda na ambaye yu tayari kukupigania hadi tone la mwisho la jasho lake!!

Kaburi nasema nawe, unisikilize umwambie Jimmy.

Mwanangu, tetesi zilipoanza kuzagaa mtaani ati ya kwamba umeshiriki penzi na msichana aliyeathirika na virusi vya UKIMWI. Nilicheka sana.

Ndio! Nilicheka kwa sababu baba yako sikuwa naujua UKIMWI kwa kiasi hicho, wewe ni shahidi namba moja kwangu, umekuwa mtoto hadi unafikia kuitwa kijana sikuwahi kukutambulisha mama mdogo. Wala hukuwahi kumwona hawara sembuse msichana akiwa na mazoea nawe kupitiliza.

Niliamini UKIMWI unawakumba wanaume wajinga tu.

Sikujua kama mwanangu Jimmy nawe ni mwanaume mjinga!

Nisamehe kaburi! Nimemwita mwanangu mjinga ilihali mimi babaye ndiye mjinga kupindukia.

Ulipoanza kuugua Jimmy nikawasikiliza marafiki wachache sana, wenye akili kama zangu wasiojua lolote kuhusiana na gonjwa hatari la UKIMWI. Wakanisisitiza tena kwa kunong’ona ili watu wasisikie.

Wakasema umerogwa na wale wanawake wa mtaani kwetu. Wakanipeleka katika tiba za kienyeji.

Naam! Huu ukawa mwanzo wa kukupoteza mwanangu wa pekee.

Mara mganga aseme unatakiwa kuishi kwake kwa siku saba akutibie. Nikakuacha kule huku nikimpatia pesa nyingi.

Siku saba zikipita ananiagiza kuku mweupe, mbuzi mweusi na makorokoro mengine ambayo siyakumbuki.

Niliagizwa hadi ile siku ninaagizwa kuuchukua mwili wako baada ya Yule mganga kusema jini ulilotupiwa ni kali sana, haliwezi!

Wale marafiki walionishauri kwenda katika tiba hizo wakanikimbia nikabaki peke yangu.

Mimi peke yangu, bila pesa wala mtu yeyote wa kunitia moyo. Nikahangaika nawe Jimmy. Mwili wako haukuwa mzito, ulikuwa umekwisha! Ulikuwa kama kitoto kidogo.

Nikazunguka huku na kule hadi nikafikia hatua ya kukupeleka hospitali.

Na hapo ndipo nikabebeshwa mzigo wa lawama. Lawama ambazo hadi leo zinaniandama Jimmy.

Nikaitwa mpuuzi, nikaitwa goigoi.

Lakini haya yote yalikuwa ya kawaida. Jitihada za madaktari zilipogonga mwamba nikaitwa muuaji.

Ati nilishiriki kifo chako mwangu.

Jimmy! Najua waweza kuwasikia wasemayo, lakini naomba usiwaamini walimwengu hata chembe.

Ni kweli walinikanya juu yako, lakini mbona hawakuwakanya wanao wasishiriki nawe anasa hizo.

Sikukuzaa ukiwa mwathirika Jimmy, kuna mmoja alikuambukizwa aidha makusudi ama bila kujua.

Yote haya hayana maana kwa sasa tena.

Umekufa mwanangu umeniacha katika upweke mkubwa sana.

Nasema nawe Jimmy nasema nawe kupitia kaburi lako.

Nisamehe kaburi!

Nisamehe kwa sababu nilifanya makosa pasi na kujua ni makosa.

Nilikulinda sana mwanangu lakini pale niliposahau kukulinda ndipo nilipoibariki safari yako hii.

Kilio hiki na kiwafikie wazazi wenzangu, yaliyonikuta mimi kukupoteza Jimmy yasiwakute na wao.

MWISHO!!

Leave a Reply