DAKIKA CHACHE KABLA YA KIFO CHANGU

Nayaandika haya huku mtiririko wa matukio mengi yaliyotokea baina yangu na wewe yakigonga kichwa changu. Nakumbuka wakati ambapo tukiwa pale chuo kikuu cha Dar es Salam, wakati ambapo tukiwa ni vijana wenye matarajio makubwa sana siku za usoni.
Ukiachilia mbali ukata, ucheleweshwaji wa fedha za kujikimu sanjari na lapsha za kila siku tukiwa pale Mlimani, hayo hayakukufanya uangukie kwa mapedeshee kama ilivyokuwa kwa baadhi ya wanafunzi wengine wa kike.
Urembo wako hukuugeuza kuwa mradi wa kujipatia fedha. Ni wewe uliyenifundisha kuwa penzi halinunuliwi kwa fedha, ulisema mtu anaweza kununua mwili kwa thamani ya pesa vile awezavyo lakini siyo moyo wa mtu, wakati wote ulisisitiza kuwa unahitaji penzi la kweli kutoka kwangu, ukaongeza kuwa furaha na faraja ndiyo mambo muhimu kwenye maisha yako.
Tangu wakati ule nilikuweka sehemu muhimu ndani ya moyo wangu, nafsi yangu ilikiri kuwa wewe ndiye mke wa ndoto zangu, ilikuwa ni fahari kuwa na mwanamke mwenye akili na fikra pana kama wewe.
Tulimaliza mwaka wa kwanza salama, tukaingia mwaka wa pili, na hatimaye mwaka wa tatu. Nauchukia mwaka ule wa mwisho wa masomo yetu pale chuoni, kwani ni mwaka niliopoteza dira ya maisha yangu.
Mambo yote haya yalisababishwa na wewe Salma, Mambo yalianza kuvurugika pale ulipoanza tabia ya kutoka ‘out’ kila mwisho wa wiki, Lucy na Mayasa walizishika akili zako vile watakavyo, mlienda disko, mkanywa pombe, mkavuta sigara na kucheza muziki huku ukishikwashikwa kiuno na walevi, Kwakweli tangu siku ya kwanza nipate taarifa juu ya tabia hizo mpya, niliuzunika sana, kimsingi ni kwamba sikukubaliana nazo kabisa.
Ukinzani baina yangu na wewe ukanzia hapo, yule Salma niliyekuwa nikimjua hukuwa wewe tena, uligeuka na kuwa kiumbe wa ajabu sana, nilijipa moyo kuwa huenda ni shetani amekupitia….hata hivyo nilichoka uliponihakikishia kwa mdomo wako kuwa huna shetani wala jini anayekutuma kufanya uyafanyayo…ukasema unayatenda kwa usimamizi wa utashi wako ulio sahihi.
Nikikaa na kufumba macho taswira ya lile tukio la fumanizi linapita akilini mwangu, aise siwezi kusahau siku nilipokufuma sebuleni kwako mkiwa mnafanya mapenzi wewe na yule Mhadhili kijana wa idara ya Lugha na fasihi ya kiswahili wa pale chuoni…. Iliniuma mno,.. sikuwa na la kukufanya siku ile zaidi ya kuchukua maji ya baridi ndani ya jokofu na kukumwagieni kisha nikaondoka nikiawaacha mkitapatapa kwa kihoro.
Nililiumia mno, na nilikuchukia, ajabu ndani ya chuki hiyo kulikuwa na sauti fulani iliyoniambia bado moyo wangu unakuhitaji, sauti hiyo ilikuja kama masikhara na kugonga kichwa changu, taswira ya sura yako nzuri ikawa haibanduki akilini mwangu, nikawa nalikumbuka penzi lako tamu la nyuma, bila kutegemea nikajikuta nakumisi.
Nilikufuata na kukuomba tusahau ya nyuma na tuanze upya, ulinikatalia salma!!!… nikakukubebelenza na kukuomba msamaha kana kwamba ni mimi ndiye niliye kukosea. Na baada ya kukubembeleza muda mrefu hatimaye ulinikubalia….tukarudiana!!.
Tangu siku hiyo nimegeuka kuwa mtumwa wa mapenzi juu yako, nafsi yangu ilikiri kabisa kuwa wewe siyo mwanamke sahihi kwangu, lakini ajabu moyo wangu ulikuwa mgumu kubanduka kwako.
Penzi lako lilitafuna mwili wangu na kubaki mifupa, nikawa kichekesho, uliniburuza vile ulivyotaka kwakuwa ulijua kwako sijiwezi, kweli nilikuwa sijiwezi mama…nilikuwa sijiwezi hata metahali isemayo kila mchuma janga hula na wa kwao. Nikaisahau!!.
Ghafla, ulianza kuugua kikohozi cha mara kwa mara, ukaharisha na kutapika, tetesi zikaanza kuzagaa kuwa umeukwaa Miwaya!.
Siku niliposikia uvumi ule, niliogopa mno, niliamini janga hilo lipo kwangu pia, nikakaza roho na kwenda Angaza kupima.
Salma ninapo andika maneno haya nipo hoi kitandani kutokana na tatizo la shinikizo la damu nililolipata baada ya kupokea majibu yangu kwenye kituo cha Angaza.
Majibu yalionesha naishi na mammbukizi ya virusi vya Ukimwi, Umeniua Salma, ndoto zangu sasa zimegueka na kuwa historia ambayo sina pakuisimulia.
Nipo hapa kitandani machozi yakinitoka, taswira ya mwisho wangu inagonga kwenye ubongo wangu, kila dakika nafikiria sehemu iitwayo mochwari, nawaza mwili wangu utakapohifadhiwa kwenye majokofu yenye baridi kali, zaidi ya yote nalifikiria kabuli langu. Kwakweli moyo wangu udhooful-hali.
Sitaki kukulaumu wewe Salma wala Sina cha kukufanya, huu ulikuwa ni uhayawani wangu mwenyewe, madhila haya kwa sasa ni yangu mimi na wazazi wangu pekee. zaidi ya yote niseme tu nimekusamehe ingawa sintakusahau.
Mwisho:
JIFUNZE:
Ziko nyakati MUNGU huvunja miili yetu ili kuokoa roho zetu, nyakati zingine huvunja mioyo yetu ili atufanye upya, mara nyingine huruhusu maumivu ili kutuimarisha zaidi. Na anaweza kutuletea kushindwa yale tuyapendayo ili tujifunze kunyenyekea, wakati mwingine anaweza kuondoa kila kitu kwetu ili tujue thamani ya alichotupatia , twapanga mipango mingi lakini ukweli ni kwamba twaishi kwa Neema ya MUNGU tu.Na si kila tushindwalo kwamba MUNGU ametuacha hapana nikipimo cha imani zetu.. Mpendwa haijalishi mapito gani unayopitia Mungu atabaki kuwa Mungu. Mwite yeye ktk shida zako.

Leave a Reply