HOUSEGIRL

“Kwanini umenifanyia hivi mke wangu, pamoja na kukupenda kote kule lakini umenifanyia mambo ya ajabu sana….” Rajabu aliongea kwa sauti ndogo yenye kuonesha maumivu makuu ndani yake.
“Stop! Ishia hapohapo mjaa laana wewe, kwanza nani mkeo, labda useme nilikuwa hawala yako, cheo ambacho kwa sasa sikipendi hata kukisikia. Eti unanipenda, hivi unavyoniangalia mimi nina hadhi ya kupendwa na wewe, achana na mimi mwanaume suruali wewe!” Hanifa alisema kwa jazba huku akiwa ameshika kiuno chake, misuli ya shingo ikiwa imemtoka, ama hakika alikuwa amedhamiria.
“Hanifa, leo hii mimi nimekuwa mwanaume suruali, sawa sikatai kweli kwa sasa mimi ni mwanaume suruali, tena unaweza kuniita hata mwanaume boksa kabisa, sina kitu kwa sasa lakini ni wewe ndiye….” Rajabu hakumalizia alichotaka kusema.
“We we we! Koma kabisa, tena koma kama ulivyolikoma ziwa la mama yako, mimi nimekufanya nini, ni ujinga wako ndio sababu, sio mimi, ujinga ambao wewe unaiita mapenzi, mapenzi? sijawahi kupenda mimi, sijawahi kupendwa mimi, sina moyo wa kumpenda mtu, hapa inapendwa pochi, mama yangu mzazi mwenyewe simpendi itakuwa wewe, kama huna pesa hapa sepaa!” Hanifa alisema kwa nguvu zaidi sasa.
“Hanifa, inawezekana kweli kwamba huna uwezo wa kukumbuka, ila nakuomba ujaribu, jaribu kukumbuka Hanifa…ulivyokuja hapa siku ile, ukiwa mnyonge, dhaifu tena mchafu, unakumbuka ulipokelewa kwa mikono miwili tena kwa upendo mkubwa sana, na mke wangu mama Sharifa…”
“Baba, hiyo ni mwaka jana, huu mwaka mwengine, nilikuja kuomba kazi kama mfanyakazi wa ndani, nakubali ulikuwa Bosi wangu, lakini sasahivi mimi ndiye Bosi kwako, nakubali nilikuja bila nyumba, nilikuja kwa miguu toka kijijini kwetu Chamwino, lakini sasa nina nyumba na gari ya kutembelea, acha kuongelea yaliyopita. Kwa sasa…..huu mwaka mwengine baba, umenielewa baba?”
“Nimemfukuza mke wangu kwa ushauri wako mbaya Hanifa…”
“Baba, Penzi langu tamu ndilo lilikufanya umfukuze mke wako sio mimi, ni ujinga wako ambao wewe unauita mapenzi, hakuna mapenzi ya dhati dunia hii baba, kama unaamini kuna mapenzi ya dhati utagawa hadi roho yako bwege wewe!”dhati
“Nimewafukuza watoto wangu wapendwa kwa ajili yako Hanifa, kwakuwa uliniaminisha utakuwa na mimi siku zote, na tutazaaa……”
“He he he! Kikaragosi wewe uzae na mimi, unataka kunibangishia wanangu bure, ujinga wako nd’o uliokufanya uwafukuze wanao, hivi mtu mwenye akili zake timamu anaweza kuwafukuza wanae wa kuwazaa, kumfukuza mkewe eti kwa penzi la housegirl? Jitu kama hilo ndo nizae nalo…..”
“Hanifa umebadilisha jina la hati ya nyumba yangu…..”
“Ishia hapohapo babu wewe…nilikushikia bunduki ili uende kwa mwanasheria kubadilisha jina la hati ya nyumba yako, si wewe mwenyewe nd’o ulisema tukabadili ili uandike jina langu…Ahsante sana baba kwa hilo” Hanifa alisema huku akifanya ishara ya kupiga magoti.
“Kadi ya gari….” Rajabu hakumalizia kusema alilotaka kusema, Hanifa alidakia.
“Ulienda kwa mwanasheria kubadili jina la kadi ya gari ili kunimilikisha mimi, mapenzi tu hayo ndio yalikuchanganya toka kwa mwanamke wa Kigogo…..kwanza unaniharibia siku tu hapa, sina muda mchafu kabisa wa kuongea na wewe, nakuomba toka nje!” Hanifa alisema huku akilionesha geti kwa kidole.
“Hanifa nionee huruma nitaenda wapi mimi…sina pa kulala..” Rajabu alisema kwa sauti iliyojaa huruma.
“Nenda hukohuko walikoenda wanao na mkeo hapa toka!”
“Hanifa..”
“Jina langu, na Swalehe baba yangu”
Hanifa alisema kwa nyodo.
“Naomba…”
“We Mwituuuuu!”
Mlinzi anaingia kwa kasi akiwa na kirungu cheusi mkononi.
“Toa huyu mbwa nje!”
Mwitu anashangaa kidogo.
“We mwitu!’ Mwitu anastuka na kutekeleza agizo. Anamshika Rajabu kiunoni, anamnyanyua kiasi kwamba Rajabu anatembelea ncha ya vidole, mnyanyuo namna ile unaitwa Tanganyika jeki.
Rajabu anatolewa nje ya nyumba aliyoijenga kwa nguvu zake mwenyewe, tena kwa dharau kubwa sana, tena na mlinzi aliyemwajiri mwenyewe.
Anatolewa hadi nje ya geti na kubwagwa chini mchangani.
Chozi la uchungu linamdondoka mchangani, analitazama geti la nyumba yake, anapangusa kamasi kwa mkono wake wa kushoto.
Mara majirani wanaanza kujaa, kusaka umbea. Rajabu anaona akiendelea kulala pale chini atajaza watu, anainuka taratibu, na kwenda kusikojulikana…..
” He he he Kantangazeeeeee” kicheko kikali kinasikika ndani toka ndani ya nyumba…
Kilichoendelea mi’ sijui.

MWISHO

Leave a Reply