MCHEPUKO SIO DILI

” Baada ya kuishi kwa muda mrefu ndoa iliyokua imejaa amani furaha na mafanikio huku tukishirikiana bega kwa bega na mke wangu kipenzi hakika sikuwahi kufikiria ipo siku familia yangu itakuja kusambaratika, inauma sana , leo nimeona nishuhudie yaliyonisibu  hivyo naamini ushuhuda wangu huu utakua funzo kubwa mno kwa wengi. Iko hivi,

 Nilikuwa ninafuraha kufikisha miaka 35 ya Ndoa yangu mimi na mke wangu, kwa pamoja tulipitia mengi milima na mabonde. Mwenyezi Mungu alitubariki watoto wazuri na wenye akili, watatu wa kiume na mmoja wa kike.
Wote kwa sasa wana ndoa zao, na wana kazi zao nzuri tu, shukrani kwa mke wangu aliyewalea kwa muda mwingi zaidi na kuwakuza katika maadili ya dini yetu.
Nilistaafu katika utumishi wa umma, ambako nilihudumu takribani miaka 38 na kupata pensheni yangu (lump sum), ambacho kilikuwa ni kiasi kikubwa mno cha pesa.
Baada ya kufunga na kuomba kwa Mungu, mke wangu alinishauri kuwekeza pesa hizo katika miradi mbalimbali (portfolio investments).
Baada ya kupewa cheki yetu, tulizichukua zile pesa na kuwekeza katika biashara mbalimbali, mke wangu ninaweza kukubali kwamba kweli alikuwa ana “idea” nzuri za biashara. Kwani ndani ya muda mfupi mauzo (turnover) yalitiririka na tukaanza kupata faida (returns) kubwa sana katika uwekezaji wetu.
Sikuwahi kushika pesa nyingi kiasi kile kwa siku moja, kwani kwa siku tulikuwa tukifanya majumuisho ya hata shilingi milioni sita kutoka vitega uchumi vyetu mbalimbali.
Ghafla maisha yetu yakabadilika haraka, nikajiunga na kikundi cha wazee wenye pesa (billionaires’ club). Nilibadili magari mara kwa mara, tukanunua nyumba na kuanza kuishi karibu kabisa na mjini.
Nikaanza kualikwa kwenye tafrija muhimu za wenye pesa, ambako huko nilikutana na mabinti wadogo wazuri waliokuja kuwapoza matajiri. Marafiki zangu kila mmoja alikuwa na msichana mzuri pembeni.
Hawa wasichana walizidi kunikaribia, kila nilipokuwa katika hizo tafrija hawakuisha kunishika shika, kifua, kidevuni na kuninong’oneza kwa lugha zao laini zenye ulimbo. Nilijihisi mimi ni mfalme Duniani. Pesa haikuwa tatizo kwangu.
Nilikutana na mmoja wa wale wasichana warembo ambae ngoja nimpe jina alikuwa akiitwa Evelyn. Huyu alikuwa akinijali sana, alikuwa akinifanyia “manicure” katika kucha zangu, hukuisha kunifanyia “massage” mwilini mwangu na kwa kweli nilijikuta nikimpenda mno.
Alinipa masharti ya kama nataka kuwa nae nimfukuze mke wangu na nimuoe yeye.
Mke wangu hajawahi kunifanyia baya lolote. Alikuwa bega kwa bega na mimi katika nyakati mbaya nilizopitia. Nilipokuwa na mzigo wa madeni mke wangu alikuwa akijitahidi kunipa moyo, alikuwa akitoa hata pesa ya kimtaji chake kidogo cha biashara na kunipa mimi ili niweze kulipa madeni.
Nilimtembelea Evelyn, na kwa kuwa kweli nilikuwa nikimhitaji nilikubaliana nae kumpa talaka mke wangu na kumuoa yeye. Nilifikiria au nimuoe Evelyn awe mke wa pili ili nisimuache mke wangu ila dini yangu hairuhusu kuoa mke zaidi ya mmoja, nilipomwambia Evelyn ndo kabisa akanijia juu kuwa yeye hataki kabisa kuwa mke mwenza tena nikome kabisa nisithubutu kumuoa kama sitaki kumuacha mke wangu,
Nilirudi nyumbani na kuanza visa rasmi, nilianza kumsingizia mke wangu kila aina ya jambo. Nilianza kumchukia kutoka moyoni. List ya matatizo nikiyomsingizia ilikuwa ndefu kuanzia kumtuhumu kuwa amenenepeana na kutumia pesa za vitega uchumi vyetu vibaya.
Pia nilimsingizia kuwa anatoka kimapenzi na mchungaji wa kanisa alikokua akisali, kwa kweli nilimsingizia vingi mno ilimradi tu nitafute ugomvi nimpe talaka aondoke zake.
Ugomvi uliendelea kila siku, kiasi kwamba nikafika hatua ya kuanza kumpiga na kumweleza kuwa aondoke zake na aniache mara moja.
Wanangu baada ya kuona kuwa nimezidi kumuonea mama yao kwa kumpiga na kumfukuza mara kwa mara ambapo ilifika hatua nikamvunja mkono wa kushoto, waliafikiana kumchukua na kufungua kesi ya talaka mahakamani.
Mahakama iliamua tugawane nusu kwa nusu mali zetu zote, ila mke wangu aligoma kuchukua mali na akadai aachiwe kitega uchumi kimoja tu kwa ajili ya kujiendesha kimaisha. Nilikubali tukaandikishiana na talaka ikatoka rasmi.
Mimi huku nilifanya mpango, nikalipa mahali kwa wajomba zake Evelyn (hakuwa na wazazi) ambao niliwaona wakiwa na njaa kali ya pesa. Tulifunga ndoa bomani na kuanza kuishi kama mume na mke.
Kwa muda mfupi nilijihisi kama mfalme kuishi na Evelyn, tulikuwa tukitoka “out” pamoja bega kwa bega. Mzee na binti mdogo anayeonesha kujali! Kweli nilihisi kupendwa sana.
Sijui Evelyn aliniroga, kwani mali zote niliandikisha upya kwa jina lake.
Baada ya muda mfupi mambo yalianza kwenda mrama, Evelyn alianza kiburi, jeuri, maneno ya kashfa, nyumba ilikuwa kama kuzimu.
Ilifika kipindi Evelyn alianza kuja na vijana waliotisha nyumbani kwangu, Evelyn alikuwa akiwatumia wale vijana wanipige na kunifungia stoo, kisha yeye alilala na mmojawapo chumbani kwangu kwenye kitanda changu.
Nilihisi Dunia imeamua kuniadhibu sasa, nilimkumbuka mke wangu mpenzi. Majuto hayakuniishia. Ila nilivumilia tu na sikumwambia yeyote maana nilijua hii ni aibu kubwa kwa mtu yoyote kujua.
Watoto wangu hawapo tena karibu na mimi. Mama yao nasikia yupo salama na anazidi kustawi kimaisha huku akiwa na furaha na faraja toka kwa wanangu, wajukuu zake na Mungu.
Naandika ujumbe huu bado nikiwa katika kifungo cha ndani, Evelyn ni mmojawapo katika kundi la majambazi, ni mwanamke mzuri amayetumiwa na majambazi kuwalaghai wenye pesa, na kweli alifanikiwa kunilaghai. Hivi sasa anamiliki vitega uchumi vyangu vyote.
Najuta mno, nimetambua kuwa kila jambo na wakati wake. Mimi nipo katika masika katika maisha yangu, haikuwa na maana kwangu kuwa na mtu ambaye yupo kiangazi katika maisha yake.
Nipo tayari kuupa ulimwengu lolote ilimradi tu muda urudi nyuma. Nimetambua ni vema kiasi gani kuzeeka na mwanamke wa ujana wako.
Ninawasihi Wanandoa hata kama mtapigwa na kimbunga cha aina gani kamwe usimuache mwenza wako katika hali ngumu.
Ninafahamu ninaweza kuwa na nafasi ya kutengeneza tena na mke wangu, kwa muda kidogo nimejitahidi kuwa karibu kwa kuwasiliana nae lakini ameonekana kuwa mgumu kwangu. Anasema ameshanisamehe ila kurudi kwangu haitawezekana kamwe.
Hapa nilipo jasho lanitoka hela imekua ngumu Evelyn kazuia kila kitu mbaya zaidi nadaiwa mikopo kibao aliyonishauri nichukuege na sasa ananikana nyumba, biashara na magari yangu kazuia na anatishia kunifukuza, sura yangu sijui nitaificha wapi nahis kifungo gerezani chaninyemelea duh najuta sana.
Najuta, nimestafu vibaya mno kwa kijitakia. Sijui ni nini kinafuata baada ya hapa.”
_______________________________________
Hayo ndio yaliyomsibu Mr. Herman, yaweza kumsibu mtu yeyote katika jamii, ni mambo yanayotokea hakika hili ni funzo kubwa mno naamini litaokoa ndoa nyingi na familia zilizokua kwenye uelekeo wa kusambaratika kama hii ya Mr. Herman, chonde chonde mwanaume unapofanikiwa kumbuka ulipotoka kumbuka aliekuwa nawe bega kwa bega hadi ulipofanikiwa dunia isikuhadae ukasahau waliopoteza muda na jitihada zao pamoja na wewe katika kufanikisha mipango yako, MTHAMINI NA KUMUENZI MKEO michepuko sio dili.

Leave a Reply